Saturday, May 30, 2015

Edward Lowassa aianza safari ya matumaini Arusha



Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli leo ameliteka jiji la Arusha kwa masaa takribani manne ambapo ilikuwa ni siku ambayo kiongozi huyo alitangaza nia ya kuwania Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiweka wazi dhamira yake ya kuchukua fomu ndani ya chama na pengine kukiwakilisha Chama cha Mapinduzi(CCM) katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 25 mwaka huu.
Tukio hilo lililofanyika kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid, lilishuhudiwa na maefu ya watu.
Inaaminika kuwa haijawahi kutokea uwanja huo kufurika idadi kama hiyo ya watu katika matukio mbalimbali yaliyowahi kufanyika uwanjani hapo.
Lowassa aliwasili uwanjani hapo majira ya saa tisa ambapo alilakiwa na viongozi mbalimbali wa Chama cha Mapinduzi wa mkoa wa Arusha, pamoja na wawakilishi wa chama hicho waliotoka karibu mikoa yote ya Tanzania Bara na visiwani.
Pia viongozi waandamizi wa CCM kutoka mikoa mbalimbali walihudhuria pamoja na viongozi wastaafu wakiongozwa na mzee Kingunge Ngombare Mwilu, Balozi Juma Mwapachu na aliyewahi kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Prof Anna Tibaijuka.
Kabla ya kukaribishwa rasmi kuzungumza na wananchi, wawakilishi kadhaa wa makundi mbalimbali ndani ya CCM walipewa nafasi ya kutoa nasaha japo kwa dakika moja.
Miongoni mwa waliopata nafasi ya kuzungumza alikuwa ni mbunge machachari wa Mwibala, Mh Kangi Lugora ambaye aliwawakilisha wabunge wa CCM wanaomuunga mkono Mh Lowassa.
Katika machache aliyoyazungumza, Mh Lugora alisema kutokana na misukosuko mingi inayolikumba Taifa, ni wazi anahitajika kiongozi kama Lowassa kuweza kulikwamua taifa katika matatizo mengi yanayolikabili.
Mh Lugola alisema yeye pamoja na wabunge ‘majembe’ wa CCM, wanamuunga mkono Mh Lowassa na akaomba wananchi pia wamuunge mkono kwa kuwa ndiye mtu sahihi wa kuiongoza Tanzania kwa sasa.
Mbunge huyo wa Mwibala alisema pia licha ya Lowassa kutungiwa tuhuma mbalimbali za kumchafua, lakini bado amesimama imara na leo ameianza safari ya matumaini ya kuijenga Tanzani imara.
Baada ya salamu za wawakilishi kutoka mikoani Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Arusha Onesmo Ole Nangoro alimkaribisha Mh Edward Lowassa kuzungumza na wananchi.
Kabla ya kuanza kutoa hotuba, Mh Lowassa aliomba wananchi wasimame kwa dakika moja ili kumkumbuka aliyekuwa mbunge wa Mbinga Magharibi marehemu Kapt John Komba aliyefariki ghafla miezi miwili iliyopita.
Kapten Komba alikuwa miongoni wa wabunge machachari waliokuwa wanaunda timu ya kampeni ya Mh Lowassa.
Katika hotuba yake Mh Lowassa alianza kwa kutoa shukrani kutokana na idadi kubwa ya watu waliojitokeza kumsikiliza akisema kwamba hiyo ni mara yake ya kwanza kushuhudia umti mkubwa wa watu katika uwanja huo.
Pia alieleza kuwa alianza harakati za kuwania Ueais wa Tanzania toka mwaka 1995 ambapo amebainisha yeye pamoja na Rais Jakaya Kikwete walikwenda pamoja kuchukua fomu za Urais huku wakikubaliana kwamba kama mmoja wao atateuliwa na chama basi mwingine atamuunga mkono.
Mh Lowassa alisema kuwa aliamua kutogombea mwaka 2005 kwa kuwa alikuwa na dhamira ya dhati ya kumuunga mkono Rais Jakaya Kikwete.
Kwenye mwaka huo,Mh Edward Lowassa anasema alikuwa Mwenyekiti wa kampeni wa Rais Kikwete na aliwezesha kupatikana ushindi wa asilimia 80.
Nini kimemsukuma kugombea sasa?
Mh Lowassa amesema kuwa umasikini, na hali tete ya nchi kisiasa na kichumu ndivyo vimemsukuma kuwania Urais.
Mh Lowassa amebainisha kuwa kama atapata ridhaa ya chama chake na Wananchi, anakusudia kujenga misingi ya uongozi wenye uthubutu,usioogopa kufanya maamuzi magumu.
Mh Lowassa anakusudia kufanya ELIMU kuwa kipaumbele kikuu kwa kujenga mfumo mpya wa elimu utakaowawezesha wananchi kuweza kukabiliana na umaskini na hatimae kuliondolea Taifa sifa mbaya ya kuwa ombaomba.
Pia Mh Lowassa amebainisha kwamba atakabiliana na rushwa kwa vitendo, ataboresha maslahi ya walimu na wafanyakazi wa Sekta ya Umma, huduma za afya, pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama.
Hata hivyo Mh Lowassa hakuzungumzia kabisa sakata la Richmond lililomuondoa kwenye nafasi ya Uwaziri Mkuu miaka saba iliyopita licha kuligusia kwenye mkutano wake na wahariri wa vyombp vya habari uliofanyia mkoani Dodoma May 25.
Katika mkutano huo, Mh Lowassa alosema kuwa hahusiki na kashafa hiyo huku akibainisha kuwa ni maadui zake wa kisiasa ndio walitunga kashafa ile ili kumchafua na hatimae aachie nafasi ya uwaziri Mkuu.
Aidha akizunguza katika mkutano huo, kada mkonwe wa Chama cha Mapinduzi, Kingunge Ngombare Mwilu amesema kuwanTaifa linahitaji kumkabidhi Urais mtu ambaye ana uwezo wa kuunganisha watu pamoja na kuulea vyema Muungano.
Kingunge aliupongeza msimamo wa CCM uliotolewa na Mwenyekiti wa chama hicho Rais Jakaya Kikwete wakati wa mikutano ya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu iliofanyika mkoani Dodoma hivi karibuni kuwa chama hicho kinahitaji kuteua mtu anayekubalika ndani na nje ya CCM.
Rais Kikwete alisema kuwa Chama cha Mapinduzi kina wanachama milioni sita tu lakini wapiga kura wanakadiriwa kuwa mil 24.
Hivyo kama chama hicho kitamteuwa mgombea nayekubalika ndani ya chama pekee, wananchi wanaweza kumkataa kwenye Uchaguzi Mkuu.
Pia Rais Kikwete aliwatahadharisha wana CCM kuwa wasahau ile kuwa mgombea anayeteuliwa na chama hicho ndiye Rais mtarajiwa.

No comments:

Post a Comment