Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema
MVUA nyepesi iliyonyesha kuanzia alfajiri, jana haikuwazui mamia
ya wafausi wa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, kujitokeza kwa
wingi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, wakati mbunge huyo
alipofikishwa kusomewa shtaka la uchochezi.
Lema ambaye alikamatwa Ijumaa usiku kwa amri ya Mkuu wa Mkoa,
Magesa Mulongo, na kuwekwa rumande kwa siku tatu, alifikishwa mahakamani
saa tatu asubuhi akiwa katika gari dogo lenye vioo vyeusi likiwa na
namba za usajili T 818 AJD.
Mbunge huyo alisindikizwa na askari wawili waliovaa suti wakiwa na silaha pamoja na Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO).
Ilipofika saa nne, mbele ya Hakimu Devota Msofe, Mwendesha
Mashtaka wa Serikali, Elianenyi Njiro, alidai kuwa kesi hiyo ni mpya na
inatajwa mara ya kwanza, angeomba asome mashtaka na ipangiwe tarehe
nyingine.
Akisoma mashtaka hayo, alidai kuwa Aprili 24, mwaka huu,
katika eneo la Freedom Square Chuo cha Uhasibu, Lema alichochea utendaji
makosa na kukiuka kifungu 390 na 35 cha kanuni za dhabu sura ya 16 kama
ilivyorekebishwa mwaka 2000.
Alitaja shtaka la Lema ni kutamka maneno: “Mkuu wa mkoa
anakwenda kwenye ‘send off’, hajui chuo cha uhasibu mahali kilipo wala
mauaji ya mwanafunzi wa chuo hiki. Ameshindwa kuwapa pole kwa kufiwa na
kusikiliza shida zenu na anasema hawezi kuongea na wanafunzi wasio na
nidhamu.” Alisisitiza kuwa maneno haya ndiyo yaliyosababisha kuvurugika
kwa amani.
Baada ya kusoma shtaka hilo, aliongeza kuwa kwa upande wao
hawana kipingamizi cha dhamana na hivyo hakimu Msofe alimuuliza wakili
wa mshtakiwa, Method Kimomogolo, kama ana la kusema.
Kimomogolo alimueleza hakimu kuwa kwa vile maelezo ya shtaka
hayaonyeshi kuelekea kwenye kutenda kosa, anaomba mshtakiwa aruhusiwe
kujidhamini mwenyewe kwa kuwa ni mbunge wa Arusha, hivyo hawezitoroka.
Hakimu Devota alitaja masharti ya dhamana kuwa ni mdhamini
mmoja mwenye kitambulisho na atakaesaini dhamana ya sh milioni moja
ambapo Diwani wa Viti Maalumu (CHADEMA), Sabina Francis, aliitwa na
Kimomogolo akamdhamini Lema baada ya kukidhi masharti hayo.
Mara baada ya kukamilika kwa taratibu hizo, hakimu Msofe
aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 29 itakapofika kwa ajili ya kutajwa tena.
Hali mahakamani
Lango la kuingilia katika chumba cha mahakama hiyo lilikuwa
na askari sita ambapo watatu walivalia mavazi rasmi wakiwa na silaha na
wengine wakiwa wanaangalia kila mtu anaekaribia hapo.
Askari wengine waliovalia kiraia walikuwa ndani ya chumba cha
mahakama wakiratibu kila mtu aliyekuwemo ndani ambapo wengi waliokuwamo
ni madiwani wa CHADEMA na waandishi wa habari.
Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nasari, alikaa na Lema wakibadilishana mawazo juu ya kilichotokea.
Nje ya mahakama ambako wananchi wengi walikuwa wamekusanyika,
nako kulikuwa na askari wengi waliokuwa wamevalia kiraia.
Mbali na askari kanzu kujaa mahakamani hapo pia askari
waliovalia sare wakiwa na gari tano huku wakisheheni silaha nzito pamoja
na mabomu ya machozi walifanya doria mahakamani na maeneo ya barabara
zote za kuelekea na kutoka eneo hilo.
Kulikuwa na magari yenye namba za usajili PT 2077, PT 1076, PT
2017 na PT 1844, zote zikiwa na askari wenye silaha kati ya saba na
tisa wakizunguka maeneo yote jirani na Mahakama Kuu mjini Arusha wakati
katika Kituo Kikuu cha Polisi kuliimarishwa ulinzi ambapo hakuna gari
lililokuwa likiruhusiwa kuingia.
Lema ahutubia
Baada ya kesi kuahirishwa, wafuasi wa Lema waliandamana naye
kutoka katika viwanja vya mahakama na kupitia ofisi ya mkuu wa mkoa
wakishangilia hadi ofisi za CHADEMA mkoa.
Kutokana na wingi wa wafuasi hao ililazimu Lema kuzungumza nao katika kiwanja cha Shule ya Msingi Ngarenaro.
Aliwashukuru kwa kujitokeza kumuunga mkono na kuwasihi kuwa
kamwe wasiwe waoga katika kutetea haki zao mpaka wahakikishe nchi
inakombolewa.
Pia Lema alivishukuru vyombo vya habari kwa kuripoti ukweli halisi wa tukio na kusaidia kuepuka kubambikiwa mashtaka.
Alisema licha ya kuwekwa rumande lakini imemsaidia kujua
masahibu mengi wanayoyapata mahabusu wanapokuwa sero, kwamba kuna
mahabusu wana siku 26 hadi 40 hawajafikishwa mahakamani.
Alisema ameshangazwa kukuta chumba cha kukaa watu 20 wanalazwa
watu 90 kitendo ambacho alidai kinahatarisha usalama wa mahabusu.
Lema alisema kuwa hatokwenda bungeni wiki yote ili apate muda
wa kufanya mikutano ya hadhara huku akiwasisitizia wananchi wa Arusha
mjini kumzomea mkuu wa mkoa popote atakapokwenda.
“Nasisitiza ilikuwa ni haki yake kuzomewa na wanafunzi wa Chuo
cha Uhasibu kutokana na dharau alizozionyesha alipofika chuoni hapo na
nawaambia wakazi wa Arusha kuendelea kumzomea popote atakapokwenda
jimboni kwangu,’’ alisema.
Nao baadhi ya wananchi waliozungumza na gazeti hili baada ya
Lema kuachiwa walimlalamikia mkuu wa mkoa wakisema ametumia madaraka
vibaya pamoja na kumpotezea muda Lema wakati shtaka lenyewe halina
mashiko.
Walisema kuwa ifike wakati uwekwe utaratibu wa kuwadhibiti
viongozi kama hao wanaochezea kodi za wananchi kwa mambo yasiyo na
msingi.
Naye Nasari alimuonya Mulongo kuacha tabia ya kuwadharau
wabunge wa CHADEMA na kusema hali hiyo itamfanya ashindwe kuongoza mkoa
huu.
Katibu wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa, mbali na
suala hilo la Lema alitoa tamko la chama kuitaka Tume ya Taifa ya
Uchaguzi kupitia kwa Mkurugenzi wa Jiji kuiunganisha kata ya Sombetini
katika uchaguzi mdogo utakaofanyika Juni 16.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), Hussein Bashe, amesema
kuwa Mulongo alionyesha dharau ya wazi mbele ya wanafunzi wa Chuo cha
Uhasibu jijini Arusha na kwamba hali hiyo inapaswa kulaaniwa na kila
mmoja.
Bashe alisema kwa dharau hiyo ni dhahiri ameivunjia heshima
serikali na kuwafanya wananchi kuongeza chuki zaidi dhidi ya CCCM.
Mjumbe huyo alitoa maoni hayo kupitia ukurasa wake wa mtandao
wa kijamii wa Facebook wakati akijadili suala zima la kukamatwa kwa Lema
pamoja na uamuzi wa baraza la madiwani wilayani Nzega mkoani Tabora
kujitengea zaidi ya sh milioni 80 kwa ajili ya safari ya mafunzo jijini
Arusha na Dodoma.
Alisema watu badala ya kutumia nguvu kubwa kuwatafuta wahalifu
waliosababisha kifo cha mwanafunzi wa chuo hicho, wameamua kutengeneza
mazingira ya kumkamata Lema.
“Kaka yangu Mulongo katika hili alivyolisimamia na
kulitekeleza ameonyesha udhaifu wa hali ya juu na matokeo yake ni
kuivunjia heshima serikali ya chama chetu na kuongeza chuki,” alisema.
No comments:
Post a Comment